Life With Muhasu » You Can Win If You Want

Kuteseka Sana Leo, Sio Tiketi Ya Kufurahia Maisha Ya Kesho

Mama yangu mzazi aliteseka sana na ugumu wa maisha kabla ya kifo chake

Licha ya kufanya ibada sana toka usichana wake mpaka utu uzima wake

Licha ya kumuabudu Mungu kila kukicha tena kwa Imani kubwa

Bado alionja joto la jiwe la maisha na utafutaji kwa ujumla

Mama alipata nafuu ya maisha mwaka mmoja tu na Mungu akamchukua!

Mwaka mmoja wa kuamini kuwa anaweza kuishi na kunilea, aliamua kunichukua rasmi ili kunilea kutoka kwa ndugu

Lakini Mungu akachukua roho yake miezi miwili tu toka aanze kuishi na mimi rasmi

“MWANANGU MWAJUMA SOMA SANA, NIKIFA AU NIKIPONA, ELIMU PEKEE NDIO MSAADA NA MKOMBOZI WAKO”

Yalikuwa maneno machache sana lakini yaliniumiza mno kwenye moyo wangu

Mama aliniachia usia huo siku ya mwisho ya umauti wake pale Temeke hospitali..

Nilijua kabisa kuwa mama ananiaga na hana muda nitampoteza

Sikuwa tayari kwa hilo kwasababu mama pekee ndie mtu niliyemtazama kama sababu za mimi kuishi baada ya kukosa Baba

Mapenzi mazito kwa mama yangu yalinifanya nitokwe na machozi yasiyo na kipimo

Ukizingatia ndio kwanza ilikuwa miezi miwili tu toka mama anichukue na kuanza kuishi na mimi rasmi baada ya kupata kazi yake

Kabla niliteseka sana kuishi kwa ndugu, wakati mama hana uwezo wa kunitunza.

Hivyo maumivu yalikuwa makali sana hasa kuwaza nitaishi vipi baada ya mama kuniacha muda mfupi tu alio nionjesha raha ya kulelewa nae!

Mungu alinipa mapumziko na raha ya mama mwenye kipato kwa miezi miwili tu kisha akamchukua!

Nilihisi kabisa kuwa Mungu alidhamiria kunitesa na hakutaka niwe miongoni mwa watu wenye furaha Duniani

Huwa sitamani hata kukumbuka siku ile maana ilikuwa siku ngumu sana ambayo imeacha jeraha kubwa kwenye kumbukumbu zangu mpaka leo hii!

Haikuwa tu kupotea mama, bali kupoteza mama wa miezi 2 na mama aliye jiaandaa kupumzisha mateso ya mwanae kupitia kipato alichobarikiwa baada ya mahangaiko ya miaka mingi sana!

Mungu ni kama alinipokonya Tonge mdomoni kwangu siku ile

Matumaini yote yalipotea ndani ya sekunde chache sana

Akili iligoma kukubali ukweli na hata moyo na roho yangu ulitaka kwenda pamoja na mama yangu kipenzi

SAUFA RAMADHANI mwanamke pekee aliyegoma kutoka kwenye ndoto zangu kila nilalapo

Kauli yake ya mwisho Ndio kama mwiba kila wakati haijawahi kufutika.

Nilijifunza mengi kupitia kifo cha mama yangu mzazi

Unaweza teseka sana kwenye maisha yako miaka mingi

Baadae ukapata wasaa wa kupumzika kwenye magumu yako

Na kisha ukayaacha mafanikio yako kama yalivyo hata kabla hujayatumia wala kuyafaidi vema

Maisha na mateso ya mama yangu miaka na miaka, na muda mfupi sana aliofurahia mafanikio yake

Vimenifunza kufurahia na kutumia kidogo nilichonacho kwa ukubwa

Bila kungoja nitakachopata kesho

Kwa sababu najua kuteseka sana leo sio tikeki ya kufurahia kesho

Usingoje uwe na kikubwa kuishi maisha ya furaha

Ishi maisha yako sasa na yafurahie kwa kiwango unachotaka kabla hujafikiria furaha ya kesho.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Usisahu Kujenga Maisha Yako Binafsi, Wakati Unajenga Maisha Ya Familia Yako

Next Post

Sikiliza Sauti Yako Ya Ndani, Ina Nguvu Na Imebeba Picha Halisi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy makala hii.