
Kuna kipindi kwenye maisha yangu nilipitia ugumu mkali sana wa maisha
Hata pesa ya kula kwa siku ilikuwa ngumu sana kupata, na kukaa siku 2 mpaka tatu bila kula kabisa ilikuwa kitu cha kawaida sana!
Tumbo langu lilizoea njaa mpaka shibe ikawa kama mseto
Siku nikishiba basi hata mimi hujihisi tofauti sana maana njaa ni kama nilizoea ndio uhalisia wa maisha yangu
Mara kadhaa nilidoea chakula cha majirani na rafiki zangu na kila nilipoitwa kula sikufanya mzaha kabisa,
(hata kama nimeshiba nitajilazimisha nikiamini nafidia kabisa wakati ujao)
Kuna muda nililazimika kutembea umbali mrefu sana kufuata chakula angalau cha mlo mmoja kwa rafiki yangu aliyekuwa anaishi mbali sana na mimi
Gwamaka binti wa kinyakusya hakika Mungu amtunze zaidi
Angalau yeye alijiongeza kukaa na mwanaume bila ndoa baada ya kupigika mtaani sana
Na nilimuona kafanya maamuzi sahihi sana kwa wakati ule hata nilitamani kutafuta mwanaume nami niishi nae bila ndoa
Ila malengo yangu yalikataa na kuniongoza kwenye uvumilivu ili baadae niishi maisha ya ndoto zangu.
Hivyo Gwamaka na mchumba wake walikuwa msaada wangu sana kipindi kile
Nilijifanya naenda kumsalimia Ila lengo kubwa ilikuwa angalau kula mlo mmoja wa siku na mara nyingi nilikuwa najichelewesha kurudi kwangu ili nile mlo unaofata kabisa bila wao kujua.
Siku moja nikiwa pamoja na rafiki yangu (mwingine) niliyekuwa naishi nae, tulipigika kwa njaa ya siku 2 mfululizo bila matumaini ya kula kabisa
Hivyo tulishauriana kwenda kwa Gwamaka kwa lengo la kupata chakula kwake
Ubaya hatukuwa na simu kwa ajili ya mawasiliano kujua kama yupo
Hivyo tuliamua kubashiri tu kwenda bila kujua kama yupo huku tukiomba Mungu tumkute
Hakika umbali mrefu ukiongezea njaa kali, ilikuwa zaidi ya mateso makali sana
Jua liliwaka mno na hatukuwa hata na nguvu za kutembea Ila tulijikaza kwa matumaini ya kweda kupoza njaa kwa Gwamaka.
Bahati haikuwa kwetu kwani hatukufanikiwa kumkuta rafiki yetu kipenzi na majirani walisema siku ile hatorudi kabisa maana kaenda mbali kwa mama yake!
Unaweza kupata picha kwa namna gani tulipata maumivu na hali ya kukata tamaa mazima
Tuliona Dunia imekuwa chungu na tulipoteza matumaini ndani ya sekunde chache sana yani matumaini tuliyokuwa nayo awali yalipotea kama upepo
Hatukuwa na jinsi zaidi ya kugeuza na kurudi tulipotoka huku tukiumia sana na tuliambulia kuomba maji ya kunywa tu kupoza kiu kwa wale majirani.
Wakati tunarudi, njiani tulikutana mama mmoja akiwa na mwanae mdogo (wa miaka kama 2 hivi)
Mama yule alikuwa anamlazimisha mwanae kula andazi dogo pamoja na maji ya kandoro ya baridi (maji ya kufunga kwenye mfuko wa nailoni)
Mtoto hakuwa anataka kabisa kula na alilia kwa nguvu huku anakataa
Nilijikuta nasema Natamani ningekuwa kama huyo mtoto kwa wakati huu
Kwa maana nilitamani atokee mtu anipe angalau andazi tu lingepoza njaa yangu
Hata rafiki yangu niliyekuwa nae pia alisema aise yani mtoto anakataa maji ya kandoro! Tena ya baridi!
Hakika unaweza kuhisi kama utani au maigizo Ila ni tukio la kweli kabisa
Hata sisi baada ya dakika kadhaa kupitia tulijikuta tunacheka sana na kujiona kama wajinga
Yani kutamani andazi na maji ya mtoto tuliyemkuta njiani hakika ilikuwa tukio la ajabu mno kwetu Ila kiuhalisia tulitamini kwa dhati kabisa.
Tuliposogea mbele kidogo tulikuta kibanda cha mama ntilie, na tulimuona mama mmoja akitoka kibandani huku ameshikilia sufuria iliyojaa maji yenye ukoko na kumwaga barabarani,
Rafiki yangu aliniambia kwa sauti iliyojaa maumivu na hisia kali, Ona Mwajuma kuna watu wanachezea chakula!
Wakati sisi tunanjaa na tunateseka kama hivi (aliongea kama vile anataka kulia)
Ni kweli alichosema kuwa tuna njaa! Lakini kuona ukoko uliojaa maji kama chakula cha dhati hakika lilikuwa suala kubwa sana
Niliamini kabisa tupo katika wakati usio wa kawaida na lazima tufanye jambo kujiokoa kwa jitihada za nguvu sana
Sikuwa na majibu kabisa Ila ndani ya moyo nilivuja damu haswaaaaaaa
Nilijikaza ili angalau mmoja awe faraja kwa mwingine kisha nikamsihi tukaze mwendo tufike nyumbani mapema .
Mpaka leo hii matukio yale hunijia mara nyingi sana kwenye kumbukumbu zangu
Hasa pale ninapoona mtu anakosa chakula, au mwingine anamwaga chakula
Huwa napata wakati mgumu sana kuona aliyeshiba anachezea chakula
Kwa sababu najua sana maumivu ya njaa kwa ambae hana kabisa chakula
Huwa siwezi kumyima mtu chakula kabisa hasa pale napoona kweli mtu yule ana uhitaji wa dhati,
Maisha ni fumbo kubwa sana, nyakati ngumu huja na kuondoka
Lakini pia unapofanikiwa kuvuka nyakati ngumu, usisahu wengine walio kwenye nyakati hizo.