
Kwa wale walio kulia kijijini na waliowahi kutumia jiko la kuni wanaweza kuelewa zaidi kuliko wale wa mjini,
Hivi umeshawahi kuwasha moto wa kuni masaa kibao na bado moto usiwake zaidi ya kuongeza wingi wa moshi?
Umewahi kusumbuliwa kuchochea kuni mpaka ukaanza kuhisi kulia achilia mbali machozi yanayotoka sababu ya ukali wa moshi!
Au umewahi kuchochea moto kwa mdomo mpaka ukahisi mashavu yanataka kupasuka?
Na kama unatumia mkono kupepea basi pia unaweza kuhisi mikono inatoa sugu mkononi na maumivu ya viungio!
Haya kumbuka pia ule wakati ambao una njaa kali sana lakini ukapata usumbufu wa moto kiasi ambacho mpaka chakula kuiva ukajikuta njaa pia imekata!
Sasa nadhani umewahi kupata jibu la mateso yote hayo ya jiko la mafiga kutokana na uzoefu uliopitia.
Kwa wewe ambae hujui basi iko hivi, jiko kuweza kuwaka au kutowaka wakati mwingine hutegemea ubichi na ukavu wa kuni zako!
Wakati mwingine ukubwa na uzito wa kuni sio sababu ya moto kuwaka!
Wala kujaza kuni nyingi sana kwenye jiko bado sio sababu ya kuni kuwaka zaidi au kuivisha chakula haraka!
Kinachoivisha chakula haraka ni ukali wa moto na ukali wa moto sio wingi wa kuni!
Mfano kifuu cha nazi huwa kidogo sana lakini kina moto mkali kuliko kuni za mninga
Hivyo kabla hujalaumu, kuchukia au hata kuacha matumizi ya jiko lako la mafiga basi unapaswa kuhakiki ubora wa kuni unazotumia,
Kwa sababu wakati unaenda kununua jiko la gas ili kuepuka adha ya kuni, kuna wenzako wanaenda shambani kutafuta kuni wakiamini kuwa ndio moto wa haraka na rahisi kupatikana bila kutumia gharama.
Kwenye maisha yetu pia ya utafutaji na safari ya mafanikio yoyote yale,
Kabla hujalaumu na kuchukia kitu unachofanya basi unapaswa kuhakiki ubora wa kitu chenyewe!
Kabla hujataka kuacha na kufunga unachofanya basi kwanza hakiki ubora wa maandalizi ya kitu chako
Kwa sababu ukubwa na uzito wa maandalizi sio tiketi ya mafanikio ya kitu hiko kama hakina ubora na tija kwa watu husika
Kwa maana maandalizi yanaweza kuwa madogo Ila yenye ubora mkubwa kama ilivyo kwa kifuu cha nazi kwenye jiko la kuni.
Unapaswa kuandaa maandalizi sahihi, kwa wakati na watu sahihi
Kwa sababu kuna uwezekano mkubwa ukaacha kitu ukiamini hakina manufaa kumbe wewe binafsi ndio umekosea maandalizi yake
Na kumbuka wakati unafunga hiko kitu kuna wenzako wameona fursa ya kitu chako na sasa wanakesha kujadiliana namna gani watafanya kitu hiko hiko kwa ubora zaidi
Pia usisahau kuwa ili moto kuwaka vizuri inataka muda ili kuni kushikana vyema na kutoa ushirikiano kwa pamoja na wakati unajishikiza ndio wakati ambao moshi hutoka kwa wingi!