
Ikinyesha na ukajua panapovuja, uamuzi utabaki juu yako binafsi
Kwa maana kubadili bati bovu, kuziba kiraka au kuacha kama palivyo!
Hivyo basi sio kila matatizo huja kwa lengo la kukuharibu na kukuumiza zaidi,
Kuna matatizo ambayo hupaswa kutokea ili kukufanya uwe bora zaidi ya mwanzo..
Na yapo matatizo ambayo hutokea kwa lengo la kukuinua zaidi au hata kukusogeza karibu na malengo unayotaka kufikia mbeleni,
Na pia usisahu kuna matatizo huja ili kuondoa tatizo zaidi ulilonalo (hata watu wasio kufaa ulionao) na kukupa njia bora ya kupata muafaka kwenye maisha yako au watu bora zaidi.
Nakumbuka tukio moja la miaka ya nyuma sana kuhusu Babu yangu (huyu ni Babu mdogo wa Babu aliyemzaa Baba yangu mzazi).
Babu yangu alikuwa mkorofi sana (Mungu ampe kauli thabiti) kwa maana kwa sasa hatunae tena,
Alikuwa mkali mno na kila mtu alimuogopa sana hata ilipotokea jina lake kutajwa (mfano kama hayupo mahala ikatokea mtu amemtaja kwa namna yoyote basi wengi waliogopa kuchangia mada kabisa).
Babu alikuwa Mganga maarufu sana pale kigoma kasingirima kiasi kwamba kigoma nzima walimjua na hata mikoa na nchi za jirani!
Hakuishia katika umaarufu wa jina pekee, bali tiba yake ilikuwa na nguvu sana kiasi alivuta watu wengi wakubwa wa vyeo na wazito sana kwenye siasa!
Babu alijiamini mno sijui sababu ilikuwa uganga wake au alikuwa na kitu kingine cha ziada!
Hakuna ambae alithubutu kuleta utata kwenye ukoo wetu na hata mtaa tulioishi watu waliogopa hata kukatiza enzi hizo za uhai wake.
Siku moja nilirudi nyumbani nikiwa nalia sana (nilipigwa na mtoto mwenzangu niliyekuwa nasoma nae)
Baada ya kufika nyumbani nilimkuta Babu nje kibarazani amekaa na wazee wenzake wanaongea,
Hivyo aliponiona nalia alitaka kujua shida kubwa ni nini haswa ukizingatia alivyokuwa mkorofi sana.
Baada ya kumueleza kuwa nimepigwa na mwanafunzi mwenzangu hakukubali alitaka twende wote shule ajue kwanini mjukuu wake (ambae ndio mimi nimepigwa)
Hivyo tulienda shuleni na Babu akapewa habari kamili, habari ambayo ilionesha yule mtoto aliyenipiga ndie mwenye makosa.
Hivyo Babu alitaka wazazi wa mtoto yule waitwe kwa ajili ya kikao (hata Walimu walimjua na kumuogopa sana Babu yangu).
Kesho yake kweli wazazi wa mtoto yule walikuja shuleni wakiongozana na Babu wa mtoto yule pia…
Na mimi pia nilifika nikiwa pamoja na Babu yangu.
Kumbe Babu yangu na Babu wa yule mtoto wao binafsi walikuwa na ugomvi wa kibiashara (kwa maana wote walikuwa waganga) ndio sababu yule mzee aliposikia ni kesi ya Babu yangu, nayeye alikuja japokuwa hakuwa na ulazima wa kufika shuleni.
Kikao kilifanyika na niliamini kuwa ulikuwa ugomvi mdogo na pengine ungemalizika tu ukizingatia hata sikuwa nimeumia popote pale.
Kumbe ndio kwanza kwao (Babu zetu) ulikuwa ugomvi ambao waliuhitaji sana ni kama vile walitamani siku ile ifike au chochote kitokee ili uwe mwanzo wa wao kukutana uso kwa uso na kugombana (Mafahari wawili)
Nakumbuka nilimsikia Babu yangu akisema “Siku zote nilitaka sana inyeshe ili nione wapi panavuja” na sasa pamevuja!
Baada ya kikao cha muda mrefu sana (kimsingi urefu uliletwa na marumbano ya wazee maana walikuwa na visa vyao binafsi) kikao kiliisha na kila mmoja alirudi kwake ila wazee wale (Babu yangu na Babu wa mtoto yule mwingine) waliahidiana kuoneshana zaidi wakikutana kwenye anga zao!
Sijui nini kilitokea lakini ukweli ni kuwa ugomvi wangu ulileta furaha sana kwenye moyo wa Babu na kama alivyoahidiana na yule mzee mwenzake ni kweli YALITOKEA YALIYOTOKEA.
Na huo ukawa mwanzo wa chuki kubwa sana kati yangu na familia ya yule mtoto tukiondoa chuki za Babu zetu.
Lakini pia upande wa Babu ni kama alishinda vita kuanzia kwenye ugomvi wangu na ugomvi wa biashara yake na yule mzee,
Kwa maana hata wateja wa mzee yule kwa kiasi kikubwa sana walihamia kwa Babu yangu, na Jina la Babu lilizidi kukuwa na kuwa maarufu sana kwenye uganga wake.
Kumbe wao kwa wao vita yao ilikuwa ya miaka mingi kwa maana ukali wa uganga baina yao ulikuwa sambamba na kila mmoja alimchua mwenzake.
Hivyo siku zote Babu aliumiza kichwa kwa namna gani atamuingia yule mzee na kumtoa katika reli na njia zake za biashara!
Kwa sababu hawakuwa na uhusiano wowote kwenye maisha ya kawaida na hata kuonana ilikuwa nadra sana (kutokana na mambo ya uganga wao na hapo siwezi elezea zaidi).
Hivyo wao kukutana siku ile ilikuwa fursa kubwa kwa Babu na aliweza kufanya aliyokusudia na kisha kubaki kilele cha Biashara yake.