
Ni chizi pekee ambae atavaa viatu vyeupe kisha kuamua kwa hiari yake kukanyaga matope.
Ni mara chache sana kutokea pale mtu avaapo viatu vizuri (brand) au hata vya gharama kubwa kiasi, kisha kuamua kupita sehemu mbaya (zenye maji na matope)
Lakini pia ni aghalabu sana kukuta mtu aliyevaa viatu vizuri maeneo ya kawaida (uswahili) au hata yasiyo na thamani kubwa…
Vilevile hutokea mara chache sana kuona mtu aliyevaa viatu vizuri akipanda daladala au hata kutembea kwa mguu! Angalau ataona umuhimu wa bajaji au boda boda kama hana uwezo wa tax,
Sio kwamba mtu huyo ana maisha mazuri sana kiuchumi, ila tu kanuni ya viatu vizuri bila yeye kuamua au kutarajia (automatic) humuongoza njia na sehemu sahihi yakupita!
Wakati mtu huyo huyo siku akivaa kiatu chochote ambacho hakina thamani kubwa basi huamua kupita popote pale…
Mtu akivaa ndala (kandambili) anaweza kupita hata katikati ya matope!
Mtu akivaa yebo yebo wala haoni shida kukanyaga hata maji machafu njiani!
Mtu akivaa kiatu kisicho na mvuto, huweza kwenda eneo lolote lenye watu wa hadhi ya chini bila kuhofia chochote.
Lakini mtu huyo huyo akivaa kiatu cha thamani na chenye mvuto basi hujiona hafai kuwa miongoni mwa aina fulani ya watu ambao kimuonekano hawana uchumi mkubwa kama anavyoamini.
Kadiri thamani ya kiatu inavyopanda ndivyo thamani ya maeneo ya mvaaji kiatu hupanda!
Kadiri kiatu kinavyokuwa na gharama kubwa ndivyo mvaaji huchagua sehemu maalumu za kuvaa kiatu hiko!
Kiatu kizuri humuongoza mvaaji aina ya maeneo na watu wa kukutana nao.
Hivyo anza kuchagua kiatu sahihi kama unataka maisha ya thamani sawa na ile unayoina kwenye akili yako!
Mwenza sahihi atakupa muongozo wa maisha sahihi na yenye thamani kubwa,
Marafiki sahihi watakupa muongozo wa maisha sahihi na maisha yenye hadhi kubwa,
Nguo sahihi zitakupa muonekano sahihi na muonekano wenye hadhi kubwa,
Eneo unaloishi sahihi pia litakupa maisha na watu sahihi.
Umakini unaopataga kwenye kuchagua maeneo ya kupita wakati umevaa kiatu sahihi, kizuri, chenye mvuto na gharama ndio umakini ambao unapaswa kuwa nao wakati wote unaochagua maisha sahihi unayotaka na unayotabiri kuwa nayo mbeleni.