Life With Muhasu » You Can Win If You Want

Jifunze Kunywa Mchuzi Wa Mbwa Ukiwa Bado Wa Moto

Mmoja kati ya mfanyakazi mwenzangu aliwahi kuniambia kauli ya “Mchuzi Wa Mbwa, Hunywewa Wa Moto”

Haikuwa mara ya kwanza binafsi kusikia Kauli hii, Ila ilikuwa mara ya kwanza kuanza kuhisi maana halisi ya Kauli hii

Nakumbuka siku hii ndio kwanza nilikuwa na mwezi mmoja pale kazini

Lakini huyu mwenzangu alikuwa na zaidi ya miaka mitatu pale kazini

Licha ya kuwa mkubwa kwa umri, cheo na hata mafanikio kadhaa, bado alinizidi uzoefu wa kazi!

Hivyo nilimpa heshima kubwa sana binafsi na tulikuwa marafiki wazuri sana kazini pale.

Hivyo siku ile tulikuwa kwenye maongezi ya kawaida tu kuhusu maisha ya kazi muda wa mapumziko na chakula cha mchana

Tukiwa Katikati ya maongezi meneja aliingia, kisha alinihitaji kwa ajili ya kumsaidia kitu fulani

Sikupinga kabisa ukizingatia bado nilikuwa mgeni pale kazini

Hivyo nilimfuata na kutimiza hitaji lake kisha kurudi kuendelea na maongezi

Ila baada ya kufika pale kwa yule rafiki yangu, ndipo aliniambia kauli ile kuwa mchuzi wa mbwa hunywewa wa moto.

Sikuelewa maana kamili na hata nilipomuuliza alikataa kabisa kunijibu

Kisha aliongeza kauli nyingine ya “asiyejua maana haambiwi maana”.

Nilipata hamu sana kutaka kujua maana halisi ya kauli ile hivyo nilianza kudadisi maisha ya pale kazini…

Na muda ulipofika nilielewa na kujifunza jambo kubwa sana,

Meneja alikuwa na tabia za kuonea wafanyakazi wageni, wale ambao bado hawamjui vema!

Tabia za kupelekeshana na hata kutumikishana nje ya majukumu yako halisi unayopaswa!

Hivyo wale wazoefu tayari walishamjua na siku zote hukataa kufanyishwa kazi nje ya majukumu yao

Ila wageni huingia kwenye mtego wa meneja bila wao kujua!

Na hapo ndio nilitafuta namna sahihi ya kuwahi kunywa mchuzi wangu wa mbwa kabla haujapoa sana

Kwa sababu kama mchuzi ungepoa kabisa basi ningeshindwa kutoka kwenye maisha na mtego wa meneja

Ningekuwa mtumwa wake na hata kuchukia kazi yangu

Na pengine ningefanya hata ambayo nisingepaswa kufanya!

Sababu ni moja tu kuchelewa kukataa mapema, kutoweka mipaka na kusimama imara kwenye haki na wajibu wangu bila kuogopa vitisho vya meneja toka mwanzo.

Hivyo unapaswa kuwahi kuweka mipaka yako toka mwanzo kwa jambo lolote, hii itakusaidia sana kuishi katika maisha unayopaswa kuishi kabla hujachelewa.

Usikubali muda upite sana kuchukua maamuzi au kukataa jambo fulani

Usiwe muoga kusema hapana au hata kuonesha hisia zako pale unapopaswa

Usijiweke nyuma kwa jambo ambalo unapaswa kuwa mbele toka mwanzo

Na hii ndio silaha ya kunywa mchuzi wa mbwa, Maana ukipoa utapoteza ladha yake

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Kitu Chochote Kile Huwa Kizuri Sana Kabla Hujakipata

Next Post

Kwenye Maisha, Hakuna Anae Wahi Wala Kuchelewa, Kila Mmoja Hupata Kwa Muda Sahihi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy makala hii.