
Kaka yangu wa tumbo moja alipo nikataa bila sababu yoyote ya msingi
“Niliumia sana ukizingatia sikuwa na mtu mwingine yoyote baada ya yeye”
Hatukuwa na Mama wala Baba, mimi na yeye tu ndio tulibaki na kupaswa kuwa kitu kimoja
Mbaya zaidi nilikuwa bado binti mdogo na ninae hitaji angalau faraja yake!
Alinikataa kabisa wazi wazi licha ya kulia sana na kumuomba msamaha bila kujua kosa langu.
Nilihangaika miaka mingi sana kuomba ndugu watupatanishe lakini kamwe hakukubali
Hata alipoulizwa sababu na watu wengine bado alisema hana sababu Ila HANITAKI TU
Haikuwa rahisi kukubali ukweli ule kamwe na wala sikukata tamaa kuendelea kujipendekeza kwake bila matokeo yoyote.
Ila siku moja nilijiuliza, ikiwa huyu huyu kaka yangu alishindwa kabisa kufika hospitali Temeke kumuona mama yake akiwa mahututi hajitambui kisa nauli shilingi mia tatu tu kutoka ubungo mpaka Temeke
Nauli ambayo hata kama ilikuwa kweli hana, bado sio point ya kuacha kumuona mama aliye kuzaa! Akiwa hoi hajitambui
Lakini kaka huyo huyo alipata nauli kutoka Dar es Salaam mpaka kigoma mwisho wa reli kuuza vitu vya mama vya urithi siku chache tu baada ya mama kufariki!
Sasa atapataje uchungu na mapenzi juu yangu kisa mimi ni mdogo wake tulio achiana ziwa?
Yani hakupata uchungu kabisa juu ya mama aliye mbeba miezi 9, akamzaa na kumlea kwa uchungu sana bila uwepo wa baba mpaka umri alio fikia
Anawezaje kunipenda mimi? Ambae sijaweza kuwa na msaada wowote kwake?
Aise yaani Mama ambae hakulala miaka nenda rudi licha ya umasikini aliokuwa nao bado alijikaza kumpa malezi bora mwanae…
Ila mwanae huyo huyo hata kuja hospitali kushuhudia dakika za mwisho za uhai wa mama yake alishindwa kwa kisingizio cha kukosa nauli!
Atawezaje kuwa na mapenzi na mimi?
Siku ile ndio ilikuwa siku ya mwisho kabisa kumtafuta hata kutaka kujua yuko wapi, anafanya nini au anaendeleaje
Na mpaka leo amenijengea uimara ambao pengine nisingekuwa nao kabisa kwa sasa
Uimara juu ya namna ya kuishi na watu! kulinda moyo wangu na kutoamini wala kutaka watu wanipe kampani zao ili mimi nijihisi mkamilifu.
Nilibaki na neno moja tu kwenye akili yangu kama kaka yangu wa damu moja amenikataa bila sababu?
Nawezaje kutaka kupendwa na watu wengine ambao hawana sababu za kunipenda?
Nawezaje kulazimisha marafiki wanipende kwa dhati ?
Naweza kulilia mwanaume tuliye kutana ukubwani anipende au abaki na mimi anapotaka kuniacha eti kisa alinitongoza?
Au nawezaje kutaka msaada kwa ndugu wengine kisa mimi ni ndugu yao?
Maisha yangu ni zaidi ya mwana jeshi… Moyo wangu ni imara zaidi ya chuma na roho yangu ni ngumu sana
Yote haya amenifunza kaka yangu hata bila yeye kujua kuwa kaandaa mtu jasiri kuliko ujasiri wenyewe huku nyuma
Pengine alihisi ameniweza na sitoweza bila yeye!
Kumbe ametengeneza kiumbe cha aina nyingine kwenye Dunia hii
Kiufupi mateso na changamoto zake zimekuwa daraja na dawa kwenye maisha yangu ya sasa..
Sababu ni moja tu sikukubali kamwe mwisho wangu mimi na yeye uwe mwisho wa maisha yangu.
Sikutaka kusimama katikati ya giza licha ya umri mdogo au ukosefu wa rasilimali yoyote
Nimepambana na maisha yangu na mpaka sasa kila hatua ngumu ya nyuma ni historia inayo nitoa machozi ya furaha na sina deni lolote wala majuto ya maisha.
Nilikubali kupambana na giza lililo mbele yangu kwa matumaini kuwa nitakutana na mwanga mbele ya safari
Na kweli mpaka sasa ninayo nguvu na uwezo wa kusimama kisha kusimulia safari yangu ilivyokuwa kwa kujiamini na kumcheka kaka yangu aliye niacha gizani wakati ule.
Usipoteze muda wako kujiona kama una makosa kisa mtu fulani
Usisimame gizani kisa kuna mtu kaondoka na tochi au mwanga wako
Kwanini usimame gizani? Au kwanini urudi ulipotoka kisa kuogopa giza?
Songa mbele kwa imani na matumaini makubwa ya kupata mwanga mwingine mbele ya safari yako
Na nina kuhakikisha utafika unapotaka, na utakutana na nuru unayotaka.