Life With Muhasu » You Can Win If You Want

Kamwe Usilale Mlango Wazi Kwa Kungoja Bahati Ya Mwingine

Huwa nashangaa sana kuona baadhi ya watu huishi kwa kukariri historia za matukio ya wengine kisha kujimilikisha au kutaka na wao wapite njia zile zile na pindi wanapokosa huanza kulaumu kwa kusema mbona fulani alipata!

Kuna watu hupata bahati ambazo hata kwa upande wao huwa miujiza tu na wengine hupita njia zilezile na mambo huwa tofauti kabisa!

Umewahi kukutana na watu ambao hufanya makosa eneo la kazi, tena hurudia kosa lile lile mara kadhaa.. mfano labda kuchelewa kazini, lakini kamwe hawafukuzwi kazi! halafu kuna ambao wakijaribu tu basi hupewa barua ya onyo au kuachishwa kazi kabisa!

Au umewahi kuona mwanamke ambae mara kadhaa amefumwa na mume wake akiwa na mchepuko ila kamwe huyo mume hamuachi mkewe! halafu kuna wanawake wakijaribu hata mara moja tu huachwa tena bila kikao cha usuluhishi wowote.

Kwenye mitaa tunaona kuna wale wezi sugu ambao hujulikana miaka na miaka kwa wizi lakini hawakamatwi, halafu kuna yule mwizi alijaribu mara moja tu akaishia kuwashiwa taili!

Binafsi ninawajua wadada ambao wameshatoa mimba kadhaa tena bila uangalizi wa daktari ila wapo salama mpaka sasa, halafu kuna binti ambae alipata ujauzito na mama yake akalazimika kumpeleka binti yake hospital kubwa sana ili atolewe ujauzito ule kwasababu alitaka mwanae aendelee na masomo nje ya nchi (walikuwa na uwezo wa kifedha) lakini binti yule alipoteza maisha chini ya mikono ya daktari!

Au mfano rahisi kuna wadada kadhaa wadangaji wazoefu ambao kupitia udangaji wao walipata waume wazuri sana wenye uwezo mkubwa na wengine (wazungu) wakaolewa kwa ndoa kabisa, halafu kuna wadangaji wengine wameishi kupata maradhi!

Kuna wale wanandoa waliokutana bar na ndoa zao zimedumu, halafu kuna wanandoa walikutana nyumba za ibada na ndoa zao hazikumaliza hata mwaka.

Nakumbuka wakati najiunga chuo kikuu na kukosa mkopo, nilipiga ruti nyingi sana kwenda bodi ya mkopo kuomba nisaidiwe ili niendelee na masomo yangu, lakini pia sikuwa mwenyewe bali tulikuwa wengi sana ambao tulikutana bodi ya mkopo na wengine kumbe walikesha pale kwa mawiki kadhaa bila msaada wowote…

Siku moja alikuja binti akitokea mkoani, akiwa na tranka (yale mabegi ya chuma ambayo wanafunzi wa bweni huwekea vitu vyao)

Yule binti alikuwa mgeni kabisa Dar es Salaam na alipangiwa chuo mojawapo jijini hapo… Alikuwa bado mshamba sana hata kwa muonekano wake tu ukiachilia mbali tranka alilobeba!

Siku hio alifika pale bodi ya mkopo baada ya kuripoti chuoni kwake na kukuta hajapata mkopo, hakuwa na uwezo wa kulipia ada kabisa hata wazazi wake kijijini walitegema apate pesa za kujikimu ili atume nyumbani ziwasaidie!

Hivyo baada ya kukosa jina lake hakuwa na mbadala wowote zaidi ya kutaka kuelekezwa ofisi za bodi ya mkopo siku hiyo hiyo ili ajue hatma yake.

Kweli wakati anawasili pale hakukaa sana mkuu wa bodi alifika pale ili kuendelea na majukumu yake..

Yule binti alimkimbilia na kupiga magoti huku akilia kwa uchungu sana (akiwa na tranka lake lile huku kavaa sketi ndefu ya kitenge na nywele za twende kilioni)

Mkuu wa bodi hakuongea kitu zaidi ya kumuuliza jina lake kisha akamwambia anamuwekea asilimia 100% za mkopo na pesa za kujikimu!

Kumbuka hakuwa yeye pekee ambae alikosa mkopo! hakuwa wakwanza kupiga magoti na kulia mbele ya mkuu wala hakuwa peke yake siku ile ambae alifika pale kwa lengo la kupata mkopo!

Ila alikuwa pekee kwa siku ile aliyobahatika kupata mkopo kwa njia ile mbele ya macho yetu ambao tulikesha eneo la bodi bila msaada wowote.

Hii iliniongezea somo kuwa bahati ya mwingine kamwe sipaswi kulalia mlango wazi!

Kama ukiamua kufanya kitu fanya kwakuwa unaamini utapata ila kamwe usifanye kwakuwa mwingine alifanya kabla na kupata.

Usifanye kosa ukijua kabisa ni kosa kwasababu uliona mwingine akifanya na hakupata madhara..

Usiingie kwenye hatari yoyote ile kwakuwa wapo walionusurika kabla, hivyo ukaamini na wewe utakuwa kama wao!

Fanya kwakuwa umetaka kwa hiari yako na unaamini kuwa njia hio itakupa kile unachotaka na kama ikiwa tofauti basi pia ni juu yako binafsi ila kamwe usifanye eti kwasababu fulani aliwahi kufanya na kufanikiwa hivyo na wewe lazima ufanikiwe,

Usiwe kama yule aliyeuza nyumba yake kisa kwenda nchi za nje akiamini atatoboa kama rafiki yake bahati mbaya akakosa visa na mpaka sasa hana uwezo wakununua hata kiwanja tena!

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Kurudisha Mpira Kwa Kipa Kwenye Utafutaji Ni Kama Matumizi Ya Boya Baharini

Next Post

Kiatu Kizuri Kitakuongoza Sehemu Nzuri

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy makala hii.