
Jambo lolote lile
Haijalishi ni jambo au kitu gani, kiwe cha gharama ndogo au kubwa
Kiwe kikubwa sana kwa muonekano au kidogo sana kwa muonekano
Kiwe kipo karibu kufikika au hata mbali sana kufikika
Au hata kile ambacho huonekana kizuri chenye kuvutia kwenye macho ya mtu yoyote
Awe Binaadamu wa kawaida, mnyama, kitu fulani au hata mazingira na nchi,
Siku zote kitapendwa zaidi na kuvuta hisia za muhitaji ikiwa bado hajakipata hususani kikiwa kwenye milki ya mtu mwingine!
Muhitaji hufanya kila anachoweza ili apate kukimiliki kwa uwezo wake wote
Muhitaji huwa tayari kujitoa kwa namna yoyote kwa lengo la kumiliki anachotaka
Atajitoa kwa nguvu zake, muda, pesa au kitu kingine chochote kile anachoweza
Lengo huwa moja tu KUPATA ANACHOTAKA!
Ila punde anapopata kile kitu, hugundua hakuna maajabu ya ziada!
Hugundua kuwa kile kitu kipo kawaida tu au hata wala hakishtui kama alivyo dhani awali
Huanza kuhisi kupotea kwa mvuto wa kitu kile kadiri muda unavyo Songa
Na kuna muda utafika kitu kile kitakuwa kama vingine vya zamani wala hakioneshi upya tena.
Na hapo hali ya majuto kwa muhitaji yule huanza kujitokeza taratibu hususani kama alifanya ambayo hakupaswa kufanya.
Hivyo kabla hujafanya kitu kibaya, kinachoumiza na kudhuru,
Fikiria zaidi kwanza na ukumbuke kuwa hiko kitu kuna siku kitapoteza mvuto wake kwenye macho yako!
Usifanye kitu nje ya malengo yako au hata nje ya sheria za Dini na nchi kisa tamaa za kupata kitu fulani
Usiharibu utu wako au hata kuacha alama ya kudumu kisa kupata kitu fulani
Jichunge na chunga wengine ukiwa katika harakati za kupata kitu fulani
Kwani msukumo wako wa leo unaweza kukupa hatari ya kudumu kesho.