
Kuna zile nyakati umeandaa kila njia na ipo sawa
Umefanya kila unachoweza na kipo sawa
Umetoa kila ulichonacho na huna ulicho bakiza
Umetumia mbinu zote na huna mashaka kabisa
Kila ulicho paswa kufanya umefanya kwa uhakika wote
Kila ulicho hitajika kutimiza umetimiza vyote
Majukumu ya upande wako yote yapo sawa na huoni kabisa kilichopungua
Kiufupi huna deni lolote wala majuto ndani yako
LAKINI HUONI MATOKEO WALA MABADILIKO YOYOTE!
Haijalishi ni kwenye kitu gani, iwe biashara kazi masomo au mahusiano au mambo mengine yoyote yale.
Basi ni wakati sahihi sasa kutumia neno LIWALO NA LIWE
Usijiumize kichwa sana wala kuwaza sana na hata kulaumu sana
Usione kama una mapungufu, huna nyota au hata una laana fulani
Usihisi kama vile umerogwa au hata Mungu amekusahau na kukuona huna maana kwake.
Kila jambo huja kwa wakati wake hivyo fanya unachopaswa kufanya na mengine acha muda uamue
Hupaswi kulaumu na kuhisi kama kuna mapungufu fulani ndani yako
Usijidhuru wala kujisababishia matatizo yasiyo na msingi wowote.
Fanya kwa kiasi chako, uwezo wako na kisha acha muda uamue matokeo yako
Neno LIWALO NA LIWE hupunguza maumivu, huondoa msongo wa mawazo na kuponya moyo wenye majonzi
Lakini pia ni dawa ya moyo na akili kushusha mzigo mzito uliobebwa kwa ndani
Ukiwa na mazoea ya kutumia neno hili mahala sahihi kwa wakati sahihi ni tiba kubwa sana na huleta mabadiliko makubwa mno kwa mtu na maisha kwa ujumla
Ila hakikisha umefanya kila ulichopaswa kufanya, Pumua kwa nguvu kisha funika kila kitu na sema neno LIWALO NA LIWE, Kisha ngoja matokeo yoyote na yapokee.