
Dunia ina kila aina ya watu ndani yake, watu wenye kila aina ya tabia haijalishi ni tabia nzuri au mbaya kwa wengine,
Mungu aliumba watu wa aina mbali mbali watu ambao hutosha kuwa kivutio kwa wengine kutokana na vimbwanga vya kila dizaini,
Hivi umewahi kukutana na watu ambao huwezi kumaliza kuwatafakari kwa vituko wanavyofanya!
Kuna wale wakubwa sana kwa umri ila hufanya vibweka kama vya watoto wadogo!
Haya ukiachana na aina nyingine zote za vibweka, kuna hili kundi la watu ambao wamechagua kunyooshewa vidole,
Wao ikitokea hata siku moja kuisha bila kusemwa vibaya au kupigiwa kelele bado huona kama vile siku hiyo haijamalizika vyema!
Watu hawa haijalishi utulivu wa wengine, wao bila kuleta ugomvi na chokochoko bado hawajaona raha ya kuishi.
Hawa hutafuta namna yoyote ile kufanya vurugu zitokee mahala bila kujali wangapi huumia!
Furaha yao kubwa ni kuona wengine wanalia, wanagombana na hata tafuruku zitokeapo.
Watu wa aina hii ni kama kwenye mishipa yao ya damu huzungukwa na sumu ya hatari muda wote,
Ni kama vile kwenye vichwa vyao kuna mlio fulani huwasumbua sana ili watafute vurugu na pindi vurugu ikipatikana basi mlio hutulia kwa muda kisha kuanza tena usumbufu!
Hawataki amani kabisa hata kwenye jambo lolote jema kwao!
Amani ni mwiko mkubwa sana na pindi amani ikitokea basi kwao ni sawa na kuvunja tamaduni za Dunia yao nyingine.
Hawa huona raha kusambaza umbea na maneno ya uongo ili mradi kuleta ibilisi katikati ya wenzao
Hawa ndio hukesha wakitunga mashauri ya namna gani watagombanisha wenzao ili wao binafsi kupata amani,
Kimsingi amani na furaha yao ipo kwenye ugomvi wa wengine!
Wakiona mtafaruku basi hukaa pembeni wakichekelea sana na hata kuona siku imeenda vyema mno wanaweza hata kula chakula kizuri au kunywa kinywaji kushushia shida za wenzao!
Na ndio hawa huongoza kwa unafki mkubwa, wakiwa na wewe hujifanya malaika ili wakuchote siri zako na kwenda kusambaza zikiwa zimeongezewa chumvi ya ziada.
Sasa ni ujinga wa hali ya juu sana kupambana na watu wa aina hii,
Kwa maana wao hufurahia vurugu na kadiri unavyo jibu mapigo bila wewe kujua, basi ndio unawaongezea siku za kuishi Duniani!
Kadiri unavyo gombana na watu kama hawa, ndio unawapa nafasi ya kufurahia maisha waliyo chagua kuishi!
Kadiri unavyotaka kushindana nao ndio kwanza wao hupata ushindi sana kwakuwa hicho ndicho haswa watakacho kutoka kwako!
Usikubali kutumika kamwe kwa watu wa aina hii, pindi unapogundua tu basi jitoe haraka kwenye mtego wao!
Nenda kinyume na matarajio yao na waone kama siku zote uonavyo maharage yakiwa jikoni, kuwa kadiri yarukavyo kwenye sufuria la moto basi ndivyo hupata nafasi ya kuiva.
Waache waishi maisha waliyo chagua kama yalivyo maharage kwa sababu yakiiva hutulia yenyewe.