
Kuna muda kwenye maisha ya utafutaji wako unapaswa kutulia kisha kuangalia mambo yanavyoenda yenyewe,
Huu ni ule muda ambao umefanya kila kitu, umeweka mambo yako sawa, umetega mitego yako yote na hata umeandaa njia zako zote katika muelekeo unaotaka!
Ule muda ambao unahisi umekamilisha kila kitu lakini pengine hujaona mafanikio uliyotarajia!
Ule muda ambao unahisi kuchoka sana baada ya kupambana mno bila mafanikio,
Ule muda ambao moyo wako unasema mbona kila kitu kipo sawa? Lakini uhalisia wa nje unakinzana na moyo!
Ule muda ambao unahisi kuelemewa zaidi, unahisi kudata au hata kukosa majibu ya wapi umekosea!
Ule muda ambao kila jambo linakuwa gumu ghafla, unahisi uwezo wa kupoteza kiwango cha kufikiri au hata nguvu za kutenda!
Ule muda ambao pengine umemaliza ufundi wako wote, pesa zako zote na hata juhudi zako zote lakini bado bila bila.
Huu sasa ni muda wako sahihi ambao kama ungekuwa baharini basi ulipaswa kutafuta boya likusaidie kuogelea!
Kuna muda ukiwa unaogelea, unaweza kuhisi kuchoka sana au hata mikono kuuma sababu ya kupiga mbizi muda mrefu…
Kutumia boya haimaanishi hujui kuogelea! La hasha pengine wewe ni bingwa wa maji au hata umewahi kushinda mashindano ya uogeleaji bora…
Ila tu kuna kipindi utatamani kutumia boya ili kukupa sapoti na hata kuhisi raha zaidi ya maji!
Boya, licha ya kusaidia kutozama kabisa ndani ya maji… Wakati mwingine husaidia kuongeza raha ya muogeleaji!
Lakini kubwa zaidi husaidia kumpumzisha muogeleaji kutumia mikono na miguu yake kupiga mbizi kila wakati..
Usisahau kuwa boya haliondoi ubora wako wa kuogelea! Wala halikupi tafsiri ya kubaki ndani ya maji milele
Bali linakusaidia kurejesha na kutunza nguvu zilizobaki kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Hivyo hata kwenye maisha ya utafutaji, kuna muda unapaswa kuacha kutumia nguvu zako kabisa…
Kisha kuangalia muelekeo wa maandalizi uliyoandaa wapi yatakufikisha.
Kwa maana kuendelea kutumia nguvu mahala ambapo hapahitaji tena nguvu.. Ni kujichocha zaidi pasi na sababu za msingi.
Kaa chini tulia acha mambo yaende yenyewe kwa muda wakati ambao unakusanya nguvu zako upya ili kurudi kwa mara nyingine ulingoni.
Huu ndio muda ambao kama kuna namna yoyote unaweza kutafuta kampani ya muda wakati unajipanga upya basi fanya hivyo..
Au kama unaweza kupata sapoti mahala popote pale, pia fanya hivyo..
Vilevile kama unaweza kujishusha kwa muda kwa mtu mwenye kuweza kukuvusha kipindi hicho pia jishushe (usiogope kurudisha mpira kwa kipa)
Na mwisho kama unaweza kuacha na kusahau kabisa kitu ulichoandaa (assume hujafanya kitu) pia fanya hivyo.
Kukaa pembeni (kutafuta msaada wa muda) haimaanishi kuwa wewe ni mjinga, mvivu wala mshindwaji
Bali hii humaanisha unajua unachofanya na unaelewa umuhimu wa mapumziko baada ya maumivu ya muda mrefu.