
Ni rahisi sana kutamka chochote kile kutoka kwenye kinywa chako
Unaweza kutamka chochote, kwa mtu yoyote na wakati wowote ule kutokana na matakwa yako binafsi,
Lakini ni ngumu sana kufuta kumbukumbu za maneno yako kwenye mioyo na akili za wengine
Unaweza kuomba msamaha na ukasamehewa Ila kamwe msahama haufuti kumbukumbu ya maneno yako kwenye mioyo ya wengine
Mdomo na ulimi ni mwepesi sana kuongea chochote kile kinachokuja kutokana na hisia ulizonazo kwa wakati huo lakini kamwe huwezi badili kumbukumbu za maneno yako kwa wengine.
Kabla hujaongea au kuropoka chochote unapaswa kufikiria madhara yake kwanza
Usijifiche kwenye kivuli cha msamaha kwa sababu msamaha sio ufitio wa madhara ya maneno yako
Unaweza kusamehewa kwa maneno lakini ukaacha alama mbaya sana kwenye mioyo ya wengine
Maneno hayarudishiki mdomoni kwa maana kwamba ukisha ongea tayari umeongea!
Na pia maneno ni ishara ya kile kilicho kujaa kwa ndani yako,
Ni bora umuadhibu mtu hata kwa viboko kuliko kauli mbaya kwa sababu ukali wa maneno mabaya hushinda hata ukali wa upanga!
Kukaa kimya sio ujinga na kamwe huwezi kuchekwa au kuharibu kisa ukimya
Ni bora ukae kimya kama huna kabisa kitu cha kuongea hususani kitu kinacho jenga mahusiano na kuboresha!
Ni bora uonekane mbaya kwa kukaa kimya kuliko kujenga ubaya kisa kauli zako
Hakika ulimi ni adui mkubwa sana wa mtu binafsi, hivyo chunga sana ndimi yako
Licha ya ndimi kuonja ladha ya vyakula, pia kazi nyingine ni kujenga au kubomoa mahusiano na wengine
Uhuru wa kuongea usikufanye ujutie majuto makubwa baadae
Uhuru wa kusema chochote usikufanye uvunje heshima yako
Uhuru wa kutamka chochote usikupe uadui na watu pasi na sababu za msingi
Lakini pia uhuru wa kuongea unaweza kutabiri kiwango cha mafanikio yako ya baadae
Hivyo tumia vizuri uhuru wako wa kuongea na chunga sana ndimi yako ili kujenga kesho yako iliyo bora.