Life With Muhasu » You Can Win If You Want

Shida Sio Kumshinda Adui, Shida Ni Nyumba Ya Vioo Unayoishi

Hivi unawezaje kujiita mshindi kwenye ushindi ambao asilimia kubwa utakufanya uanze upya!

Kuanza upya kwenye kitu ambacho ulikijenga kwa shida na nguvu kubwa hapo nyuma!

Na sio shida na nguvu pekee, bali kitu ambacho kitaacha wategemezi wako wazi kabisa pasi na tumaini lingine lolote la haraka!

Umewahi kujiuliza ugomvi unaoanzisha kwa sasa, Je kwa namna gani utauzima mbeleni?

Ugomvi ambao kwa sasa unakupa paniki kubwa sana na moyo unadunda kasi kwa kuwaza ushindi kwa adui yako, Je umeshajiuliza pia vipi kama ukishindwa?

Na sio kushindwa tu, je umehesabu ni madhara kiasi gani utapata baada ya ugomvi huo?

Au tuseme shida sio madhara kwa maana huogopi chochote kile, Tuongelee sasa kwa namna gani utarudi upya baada ya madhara yatakayo tokea?

Au unadhani hao wanao kuchochea sasa baada ya mambo yote kuharibika watabaki upande wako?

Hao rafiki zako ambao kwa sasa wanakupa misifa kuwa usikubali kushindwa, unahisi watabaki na wewe hata baada ya madhara baadae?

Sawa inawezekana huogopi kabisa kuhusu chochote kwa sasa bali unataka kumfunza adabu huyo mtu aliyekupa shida moyoni!,

Basi angalau waza kuhusu familia, watoto (mke/mume) na hata ukoo wako mnyonge unao kutazama kwa sasa.

Kumbuka kwenye maisha kuna muda unapaswa kuonesha umwamba wako ili kujenga heshima kwa wengine, lakini kuna muda unapaswa kulinda heshima zaidi kupitia kuepuka madhara makubwa utayopata baada ya kuonesha umwamba!

Kwa maana wakati unamcheka mtu anaeanzisha ugomvi wa mawe ikiwa anaishi nyumba ya vioo, ndio wakati huo huo unachekwa na wengine unapotaka kuchokoza moto ambao pengine hata hujui maji ya kuuzima utatoa wapi!

Jiulize tu!

Mtu unaetaka kupambana nae, unajua nguvu alizonazo nje ya nguvu za mwili ambazo unahisi kabisa hakuwezi kwa misuli yako iliyoshiba zaidi yake?

Unaweza moto wa mtu mwenye mkono mrefu nje ya sheria kuliko wewe?

Unajua watu wangapi wazito na wakubwa wapo kiganjani mwake kuliko watu ulionao wewe?

Unazijua vyema akili zake za ndani ukiondoa akili hizo unazoona anazo kuonesha kwa nje?

Unajua hasira zake pia huzimwa kwa kitu gani tukiondoa hasira zako ambazo unataka kuzizima kwa kumshinda kwenye ugomvi unaotaka kufanya?

Ni kweli sikatai unapaswa kumpiga sana, kumtusi sana au hata kulipa kisasi kwa njia yoyote ile..

Haupingwi wala kukatazwa kabisa kwa maana ni haki ya msingi!

Lakini kabla hujafanya yote hayo kaa chini hesabu na madhara yake pia,

Kwa maana uhakika wa usalama baada ya kuacha mipango yote ya ugomvi na kukaa kimya ni mkubwa kuliko uhakika wa madhara baada ya ugomvi unaotaka.

Kama unahisi unaweza kumudu hasara za madhara yote ya maisha yako na wategemezi wako pia basi endelea mbele…

Na kama unaona kabisa njia yako inaweza kuwa mbaya yenye majuto makubwa mbeleni basi hujachelewa na unaweza kuacha sasa hivi kisha kurudi nyuma!

Ni bora kuchekwa kwa ujinga na uoga wako kuliko ujanja usio na faida kwa maana kuna watu wanaweza kukuhakikishia uwazi wa mlango unapoingia ila kamwe hawatokuhakikishia uwazi wa mlango unapotaka kutoka

Bora nusu shari kuliko shari kamili.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Kuna Wakati Unapaswa Kuacha Inyeshe Ili Ujue Panapovuja!

Next Post

Nguvu Ni Kama Jua, Huwaka Sana Mchana Lakini Huzama Jioni

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy makala hii.